Wednesday, February 5, 2014

MAMBO YA MSINGI 20 YA KUJIFUNZA KUTOKA KWA HABARI YA DAUDI NA GOLIATHI 1SAMWELI 17:1-55, NA 18: 1-5.



                                                      
1.JINA LA YESU lina uwezo mkubwa kuliko majina yote. Daudi akasema nakujia kwa Jina la BWANA. Tumia jina hilo unapotaka maombi yako yawe na ushindi. 

2.Mawe matano yanawakilisha huduma tano, uchungaji, utume, unabii, ualimu na uinjilisti. Hawa wote wanatakiwa kuwepo katika kanisa na kulelewa namchungaji ndio maana ya Daudi kuweka mawe hayo ndani ya mkoba wa kichungaji.

3.Daudi alichukua mawe matano pia kwa sababu alipeleleza na kujua Goliathi ana ndugu wengine wanne wenye mwonekano kama wake (THEOLOGY). Katika hili tunajifunza kujipanga kwa changamoto za baadaye hata kama bado hazijafika. Kama leo ni shwari basi jipange kwa ajili ya Kesho. Kwa lugha ya uchumi tunasema jifunze kuweka akiba.

4.Upako wa Kwanza ulimpa Daudi nguvu ya kujihesabia mshindi hata kabla ya watu kujua kuwa yeye ni mshindi. Alitafuta kutumia nguvu yake. Usikae kimya wakati kuna jambo linaharibika na unajua kabisa unao uwezo wa kuweka mambo kwenye mstari.

5.Ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Sauli na majeshi ya Israeli walijiona wanyonge na dhaifu kwa Goliathi.(walifadhaika na kuogopa sana) lakini Daudi alijiona kuwa mshindi na kweli akamshinda Goliathi.

6.Daudi alitumia silaha dhaifu (kombea na jiwe) lakini alishinda, maana yake hata kama unahisi huna nguvu nyingi, huna pesa nyingi, huna jina kubwa, huna elimu kubwa, unadharaulika kama Goliathi alivyomdharau Daudi, Mungu akikutia nguvu, kile kidogo ulichonacho kinaweza fanya mambo makubwa saana! Efeso 3:20 Mungu hufanya zaidi hata tuwazayo na tuombayo.

7.Daudi hakutafuta umaarufu, kwa sababu kama angependa umaarufu basi baada ya kuua dubu na simba angejitangaza lakini alitulia mpaka alipokutana na Goliathi. Tena hata baada ya kumuua Goliathi ni wana wa Israel walioanza kumwimbia nyimbo nzuri zaidi ya zile za mfalme. Si yeye aliyejitangaza. Nia yake haikuwa kujulikana bali kufanya mapenzi ya Mungu. Usihubiri au kuimba ili tukujue bali fanya kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mungu. Mungu akikuinua hutapata shida ya kujitangaza.

8.Mungu huwainua watu kutoka kiwango kimoja kwenda kingine. Upako mmoja hadi mwingine. Daudi alipomuua simba na dubu ndipo alipoweza kumuua Goliathi. Unapotulia na kunyenyekea chini ya Mkono ulio hodari wa Mungu,basi Yeye atakuinua kwa wakati wake(1Petro 5:6). Muda mwingine Mungu anaonekana kama anachelewa kwa sababu tunataka kuruka hatua, katika maisha yako, Mungu anajua hatua unazotakiwa kupita, ukiisha kuua simba na Dubu Mungu atakuwezesha kumuua Goliathi. Mungu anapotaka kukuinua lazima aruhusu tatizo ambalo wewe peke yako ndo utakuwa na jibu lake.

9.Tunajifunza pia kwamba matatizo siku zote yapo tu haijalishi unafanya kazi gani. Usifikirie kwamba ukiwa mtumishi basi majaribu yanapungua.ooh, mengi tu. Popote ulipo jifunze kuwa mwaminifu na Bwana atakuinua. Daudi alikuwa mwaminifu kwa kuhakikisha usalama wa wanyama malishoni ndipo Mungu akamwamini na kumpa Taifa zima la Israel. Umeshindwa kuongoza familia yako, utawezaje kuendesha kanisa la watu mia? Umeshindwa kuongoza idara ya watu 6 unataka kuwa mkurugenzi wa kampuni ili iweje? Usije sema labda nikioa ndo nitaacha uzinzi, labda nikipata milioni mia ndio nitaacha wizi, au labda nikibadilishiwa kazi ndo nitaacha rushwa. HAPANA, tenda kwa uaminifu hapohapo ulipo na Bwana atakuona.

10.Katika kila jambo, hata kama dunia nzima watasema hili haliwezekani wewe soma LUKA 1:37. “hakuna la kumshinda Mungu” Ndio maana kaka zake walipomkebehi Daudi, yeye hakujali akamfuata Goliathi na kumuua. Vikwazo vya mafanikio yako vinaweza kutokea hata ndani ya familia yako au kwa watu wako wa karibu sana, tena wanaoonekana wenye uwezo kuliko wewe, hakuna sababu ya kukata tamaa ni mwanzo mwisho tunasonga mbele. Umetengwa baada ya kumpokea Yesu? Kaza buti songa mbele mpaka Goliathi atie amri chini.

11.Daudi hakufurahia watu wa Mungu wanapotukanwa. Kama mtu wa Mungu kamwe usifurahie watu wanapomsema mtumishi wa Mungu vibaya, hata kama ni kweli katenda uovu, endapo ni mpakwa mafuta wa Bwana kuna utaratibu wa kuyasema na si kuropoka tu. Kumbuka watu wa karibu ya Musa waliadhibiwa na Mungu kwa sababu walimsema vibaya Musa japokuwa ni kweli alikosea.

12.Vita kati ya wana wa Israeli na wafilisti vinawakilisha vita vya watu wa Mungu dhidi ya Shetani na jeshi lake na imetupasa kulishinda kwa kukaa ndani ya Neno(ujumla wa huduma tano kanisani) na kulitumia Jina la Bwana.

13.Shetani ana mikwara mingi sana. Anatumia ufahamu wetu kutufanya tuhisi kwamba yeye anaweza zaidi yetu. Goliathi alitumia muda mwingi kuwatisha majeshi ya wana wa Israeli, kama ilivyo leo shetani anavyokutisha kwamba hutapona, hutafanikiwa, utakufa, utachekwa ukiokoka nk. Daudi hakutishwa kamwe. Unapoiruhusu roho ya hofu ndani yako basi unafanyika mateka wa Shetani. Tunatakiwa kuangusha ngome za fikra zetu zipate kutii uwezo wa Jina la Bwana badala ya kuogopeshwa na matatizo. Tatizo lako ni la muda mfupi tu amini sasa na Bwana atakutokea na kukushindia.

14.Usijadiliane na adui. Wana wa Israeli walitakiwa kujipanga kuvamia, kwa mfano wangeamua watu sita wamvamie Goliathi na wengine wavamie jeshi la wafilisti wangemaliza kelele zote za Goliathi. Kitendo cha kujadiliana na Goliathi kilimpa Goliathi nafasi ya kuingiza hofu mioyoni mwao, don’t compromise with devil’s deceptions /techniques.

15.Daudi alivaa nguo za kijeshi lakini akavua baada ya kuona hazimfai. Maana yake unaweza kujaribu suluhisho/njia za mtu mwingine lakini haishauriwi kwa sababu Mungu alikuumba wewe original, unapocopy na kupaste maana yake uwezo wako na wajibu wako unauweka kuwa kipolo na ufanisi wako unaweza kuwa na matunda kidogo. Japokuwa unaweza usijue kama matunda yako ni madogo. Usiseme kwa sababu wengi wanasoma sheria au udaktari basi na mimi lazima nisome, usiseme kwa kuwa wengi wanapinga Injili basi na mi naogopa kuwa wa tofauti. Mungu alikuumba ukiwa tofauti kabisa na watu wengine, Mungu huwa hafanyi duplications. Anaumba vitu vipya. Hata mapacha wa kufanana nao wanatofauti kubwa sana. Mungu ana kusudi na maisha yako, tafuta kujua na utende vema.

16.Kuwa na umri mdogo si kigezo cha kukuzuia kufanya mambo makubwa ya ufalme wa Mungu. Daudi alikuwa na miaka 17 wakati anamuua Goliathi. Alikuwa mtoto wa mwisho na aliyedharaulika (katika sura ya 16 mzee Yese hakumuhesabu kati ya watoto wake lakini Samweli alisisitiza kama yuko mwingine ndipo Yese alipoagiza Daudi aitwe kutoka malishoni) lakini alitoa suluhisho la nchi nzima. Jitambue na kuelewa ni hazina gani Mungu ameweka ndani yako! Leo kuna milionea wengi tu ulaya ambao wana umri wa miaka ishirini, hata wewe unaweza kuwa miongoni mwao. Hii ndio sababu sioni ugumu kufundisha na kuandika masomo ya mahusiano, kwa sababu Mungu amenifundisha hata kabla sijaoa.

17.Mtu asiyetahiriwa (asiye na agano la Mungu, yaani mganga wa kienyeji, mchawi, mshirikina, kibaka, mwuaji, na wafananao na hao) hana uwezo wa kuyatisha maisha yako ukimtegemea Kristo.

18.Daudi akasema asizimie moyo mtu yeyote kwa ajili ya huyu, mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na mfilisti huyu. Nami nakuambia leo usizimie moyo kwa ajili ya jambo hilo (Ukosefu wa ajira, ugonjwa, fitina, umasikini nk) maana katika yote tunaye atushindiaye, Kristo atayamulika mapito yako na kukushika kwa mkono wake wa kuume pale tu utakapoamua kumwamini kwa moyo wako wote.

19.Daudi alimkata kichwa Goliathi kwa upanga (Neno la Mungu ni kama upanga). Kwa hiyo hakikisha unapoingia vitani una neno la Mungu la kutosha na unaliweka katika matendo, hata Yesu alipojaribiwa alitumia Neno la Mungu kwa ufasaha na akamshinda shetani.

20.Mfalme Sauli hakumwacha Daudi arudi nyumbani kwake. Unapokuwa mshindi, yaani umeleta suluhisho au kufanya jambo la kipekee sehemu fulan(kanisani, ofisini, idarani, wizarani, ndani ya taasisi nk) lazima heshima yako itapanda tu, bosi atatamani uwe assistant wake, Daudi kutoka malishoni mpaka kuishi ikulu si mchezo. Fanya vizuri sehemu uliyopo ndipo Mungu atakupeleka hatua ya juu zaidi, kuwa mnyenyekevu, mwenye bidii na mcha Mungu. 


No comments:

Post a Comment