Wednesday, November 5, 2014

KWA WAOAJI......

MWANANGU MPENDWA NAOMBA UNISIKILIZE KWA UZURI KABLA HUJAOA...

1.Mwanangu.
mwanamke anaweza kuwa mkeo,mwingine anaweza kuwa Mama watoto wako,lakini ukipata mwanamke ambaye atakuwa kama mama kwako,mama kwa wanao na mama kwa familia.tafadhari mwanangu usimuache huyo!

2.Mwanangu
Usimfanye mwanamke wako kuwa ndio wa kupika na kufanya kazi zote za jikoni peke yake,tabia hiyo siyo nzuri kwani hata ...nyakati zetu Mashamba yetu yalijulikana kwa majina yetu wanaume lakini tulifanya kazi pamoja

3.Mwanangu
Nikikwambia wewe ni kichwa cha familia,simaanishi kutuna kwa pochi lako,usiangalie kabisa pochi lako,angalia kama utaona tabasamu usoni kwa mke wako.Pesa sio kila kitu katika ndoa haileti ukuu wa familia!

4.Mwanangu
Ukitaka kuwa na maisha marefu na ukapunguza misongo ya mawazo,ongea na mkeo pangeni bajeti na mahitaji yenu,kasha mwache mkeo awe na jukumu la kuratibu mahitaji ya kila siku ya familia kwa kumkabidhi fungu husika hata kama limetokana na michango yenu wawili..
Wanawake wanajua sana kupanga bajeti na haitakuwa rahisi yeye kutumia hela hovyo,wakati akijuwa nyumbani kuna mahitaji ya msingi,lakini hela zikiwa kwako ataendelea kuomba hata kama utakuwa umeishiwa

5.Mwanangu
Usithubutu kumpiga mkeo,maumivu ya kipigo hukaa ndani ya moyo wake kwa muda mrefu sana na huacha kidonda ambacho hukawia sana kupona.Ni hatari sana kuishi na mwanamke mwenye majeraha moyoni

6.Mwanangu
Sasa unaamua kuoa,kama bado utaendelea kuishi maisha kama ya ubachela na mke wako,sio muda mrefu utakuwa bachela tena.Ukioa badilika anza kuishi maisha ya mke na mume.

7.Mwanangu
Zamani tulikuwa na wake wengi na watoto wengi kwa sababu tulikuwa na mashamba makubwa na mavuno yalikuwa makubwa,lakini kwa sasa maisha yamebadilika,kwa hiyo mkumbatie mwanamke wako peke yake kwani hakuna ardhi tena na mahitaji ya watoto ni makubwa sana.Angalia ukubwa wa familia yako!

8.Mwanangu
chini ya mwembe ambao nilikuwa nikikutana na Mama yako inaweza kuwa ni hoteli kubwa nyakati zetu,lakini kumbuka kitu pekee tulichoweza kufanya chini ya mwembe ilikuwa ni kukumbatiana pekee,Nakushauri ukikutana na marafiki wa kike kikubwa unachoweza kufanya nao ni kupeana mikono na ikizidi ni kukumbatiana hadharani na si vinginevyo.

9.Mwanangu
Usibadilike mara utakapoanza kupata mafanikio zaidi kuliko kuwahudumia hao viruka njia wa mtaani ambao hawajui mmetoka wapi na mkeo nakushauri utumie na kufurahia mafanikio yako na mkeo ambaye aliweza kusimama imara wakati wote wa mapito yenu magumu

10.Mwanangu
Kumbuka unapoanza kusema au kuona mke wako kabadilika,ujue kuwa kuna kitu ambacho ulikuwa unakifanya umekiacha kukifanya.Jitathmini na anza kufanya au kutimiza wajibu wako

11.Mwanangu
Usijaribu kumfananisha au kumlinganisha mke wako na mwanamke mwingine wa nje,kwani hata yeye anakuvumilia sana na hajakufananisha na mwanaume mwingine yoyote huko nje na ndio maana aliamua kuwa na wewe.

12.Mwanangu
Sasa hivi kuna hiki kinaitwa haki za wanawake,ni sawa kama mwanamke anasema ana haki sawa na wewe katika nyumba basi gawanya mahitaji yote ndani kwenu katika sehemu mbili zilizo sawa,halafu timiza nusu yako na mwambie atimize nusu iliyobaki

13.Mwanangu
Nilimuoa Mama yako akiwa bado kigoli (Bikra) na nilikuwa naenda sana kwao kabla sijamuoa,lakini kutomkuta mkeo bikra kusikufanye umalaumu kuwa alikuwa muhuni kumbuka,wanawake wa Enzi zetu na wasasa ni tofauti,ulimchagua mwenyewe, na ukigoli hukuujua kabisa.Usiingize mambo ya kabla ya ndoa kwenye ndoa yenu.

14.Mwanangu
Sikuwapeleka Dada zako shule kwa kuwa nilikuwa njinga kama wazee wengi wa hapa kijijini wasemavyo,tafadhari usifanye ujinga huu,kwani kiwango cha mafanikio ya wanawake wa sasa kimefanya wanaume waonekane ni watu wa kawaida sana na sio muhimu kama Enzi zetu.Ukijaliwa watoto wape elimu.

15.Mwanangu
Zamani Enzi za ujana wetu,wanawake walikuwa na urembo wa asili,ingawa siwezi kukudanganya,wengine waliongeza urembo kwa kujichora hina na hata kutoboa pua na masikio lakini usisahau hawakuonesha maumbile yao na nyeti hadharani

16.Mwanangu
Mama yako na mimi hatuna hisa katika kila kitu kinachoendelea katika maisha yenu,Jaribuni kutatua changamoto zenu wenyewe bila kila mara kuja kwetu kuomba usuluhishi.Ndoa ni pamoja na ukomavu wa kutatua changamoto zenu bila kuziuza kama gazetini kwa kila mtu.

17.Mwanangu..
Nilimnunulia mama yako kifaa cha kupikia vitumbua ili aanzishe mradi wa kuuza vitumbua,pia nilimsaidia kununua cherehani yake ya kwanza,Tafadhari msaidie mke wako kutimiza ndoto zake kulingana na uwezo wako kama ambavyo unahangaika kutimiza ndoto zako

18.Mwanangu usiache kutusaidia mimi na mama yako,utu uzima una changamoto nyingi sana na Mungu akikujalia utaziona muda ukifika.Pamoja na kutimiza majukumu yako kama Baba wa familia kumbuka pia bado tunaishi na wewe ni motto wetu.

19.Mwanangu...
Kila upatapo muda wa kuomba,omba na familia yako,kuna kesho ambayo huijui,ongea na MUNGU wako ambae anajua kila kitu kila siku

20.NAKUTAKIA MAISHA MEMA YA NDOA MWANANGU NAKUPENDA

No comments:

Post a Comment